Thursday, 11 June 2009

BAJETI YA TANZANIA 2009/10 YASOMWA LEO BUNGENI

Bajeti ni Tegemezi kwa 30%
Taasisi za kidini kuanza kulipa kodi
Walevi na wavuta sigara wazidi kubanwa
Wizara ya Elimu yapewa kipaumbele
Matumizi ya serikali yazidi kwa 30%
Mapato hayaridhishi
Wafugaji wasahauliwa
Zanzibar yapata 4.5% ya bajeti
Wananchi wajiuliza, Je, Kweli Itawasaidia
Ni Nini maoni ya wananchi na viongozi wengine kuhusu bajeti hii?


Tulisubiri tangu zamani,tangu tukisikia sera za maandalizi ya bajeti ya mwaka huu wa 2009/10 ambapo mambo mengi yalifanywa na serikali ili kuhakikisha kwamba bajeti inakwenda sambamba na matakwa ya Watanzania wote, wengi wao wakiwa masikini.Bajeti hii imesomwa leo ikiwa imeatanguliwa na hotuba ya Rais wa Jamhuri wa Muungano hapo jana alipokuwa akizungumza na wazee wa Dodoma pia watanzania wote katika ukumbi wa Kilimani ambapo jambo kubwa alilozungumza ni kuhusu madhara ya mtikisiko wa uchumi duniani.Kiufupi ni kwamba hotuba hiyo iliwavutia wengi.
Sasa turudi katika suala letu la siku ya leo,suala nyeti ambapo leo mida ya saa kumi jioni tumemshuhudia Waziri wa Uchumi Tanzania Mhe.Mustapha Haidi Mkulo akifungua mkoba na kutusomea bajeti hiyo.Tuache longolongo shuhudia mwenyewe hapo chini angalau muktasari au wazungu wanasema 'summary' ya bajeti hiyo

SEKTA -MIUNDOMBINU Sh.1.1 Bilioni Ikiwa ni ongezeko la 12%
-KILIMO Sh.667.0 Bilioni ongezeko la 30%
-MAJI/UMWAGILIAJI Sh.347.3 Bilioni ongezeko la 50%
-NISHATI/MADINI Sh.285.5 Bilioni pungufu kwa -24.6
-ELIMU Sh.1.74 Trilioni ongezeko la 22%
-AFYA Sh.963.0 Bilioni ongezeko la 5.7%

MAELEZO MENGINEYO
MAPATO YA NDANI NI SH.TRILIONI 5.1
MATUMIZI YA SERIKALI NI SH.9.5 TRILIONI-Ikiwa ni ongezeko la 30%
KUDHIBITI KUYUMBA KWA UCHUMI SH.1.7 TRILIONI
WAHISANI SH.3.8 TRILIONI
BAJETI TEGEMEZI KWA 34%
MENGINEYO 1.2 TRILIONI

MAONI YA WATU MBALIMBALI KUHUSU BAJETI HII
Profesa Ibrahim Lipumba "uwazi unahitajika katika katika ulipaji wa makampuni,tusije kupata EPA ya pili manake bajeti inaweza kupangwa halafu utekelezaji ukawa sifuri". Pia Prof.Lipumba aliongeza kwamba bajeti hii haijamzingatia mtanzania wa kawaida yaani masikini, "masikini hawafaidiki na bajeti hii badala yake mabenki ndo yatakayofaidika na bajeti hii".
Said Kubenea "Ni kweli fedha zimetengwa lakini hatuna uhakika na utekelezaji huko mawizarani,yanweza kuzaliwa 'Marichmondi'mengine huko na yakalipwa fedha hizi".
Ole Sendeka-Mbunge wa Simanjiro "inashangaza kuona kwamba bajeti imekumbuka wakulima tu,wafugaji je? Bajeti hii imewasahau kabisa wafugaji wa kawaida kama wa kule Simanjiro watafaidika nini na bajeti hii? Halafu pia inashangaza kuona hata taasisi za kidini zinatozwa kodi ya VAT,hili limetushitua wengi sana".
John Cheyo-Mbunge wa Bariadi-"suala la madini limefumbiwa macho kabisa,tuliunda tume tukatoa mapendekezo lakini hakuna hata moja lililofanyiwa kazi.Wakubwa katika migodi wameendelea kulindwa na kuogopwa na bajeti hii".
Aidha katika hali ya kushangaza taasisi za dini ambazo zimekuwa zikitoa mchango mkubwa sana katika maendeleo ya nchi eti! nazo zitaanza kutozwa kodi katika baadhi ya huduma 'isipokuwa huduma za kiroho'.Hata hivyo jambo hili limewakera wengi na kushangazwa na kauli hii katika bajeti ya mwaka huu.Wengi hawajalipokea suala hili katika mtazamo chanya na wanasubiri kuona Bunge litachukua hatua gani wakati wa kujadili na kuiptisha bajeti hii wiki ijayo.Ikiwa ni hali nyingine ya kushangaza,waziri Mkulo amesema kwamba msukumo umewekwa zaidi katika kilimo wakati bajeti inaonesha kwamba ni sh.667.0 Bilioni tu zilizoelekezwa katika wizara hiyo.
Haya sasa wewe je,mwananchi wa kawaida una maoni gani kuhusiana na bajeti hii?
Je,kweli unaona itakusaidia?
Tafadhali tupe maoni yako.

Na Frank Joram
Mwandishi wa makala hii
11/06/2009

No comments: